Alhamisi 4 Desemba 2025 - 13:45
Je! Ni kwa Sababu Ipi Wino wa Wanazuoni Unepewa Uzito Mkubwa Kuliko Damu ya Mashahidi?

Hawza/ Amirul-Mu’minin Ali (a.s.) anaiona elimu kuwa ni urithi wenye thamani kubwa mno; na kwa hakika, urithi huu hauwezi kulinganishwa na jambo jingine lolote katika Uislamu.

Shirika la Habari la Hawza - Amirul-Mu’minin Ali (a.s.) kuhusiana na thamani ya elimu katika Nahjul-Balagha anasema:

«الْعِلْمُ وِرَاثَةٌ کَرِیمَةٌ.»

Elimu ni mirathi yenye thamani. (1)

Sherehe:
Huenda ikasemwa kuwa; mtazamo na uangalizi maalumu uliopo katika Uislamu kuhusiana na elimu na kujifunza, hauonekani kwa kiwango hicho katika mambo mengine. Sababu ya hilo inaweza kufupishwa katika kauli hii: “Kinyume cha elimu ni ujinga; na ujinga ndio chanzo cha upotovu wote.”

Silaha inayomtoa mwanadamu katika ujinga na kumwelekeza katika amri za Mwenyezi Mungu ni elimu na maarifa. Elimu na maarifa ambayo tusipozipamba nafsi zetu na vitu hivyo, tutakuwa ni chombo cha kuchezewa na kufanyiwa matumizi mabaya na fikra za watu wasiofaa; kwa sababu hapo hakutakuwepo tena na irada. Irada ambayo ilitokana na upatikanaji wa elimu na maarifa.

Riwaya zitakazotolewa hapa chini zinaonesha kwa uwazi nafasi ya pekee kabisa ya elimu na kujifunza:

Kutembea mwenye kutafuta elimu juu ya mbawa za malaika

Katika hadithi yenye mazingatio makubwa, Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) anasema:

«إِنَّ اَلْمَلاَئِکَةَ لَتَضَعُ أَجْنِحَتَهَا لِطَالِبِ اَلْعِلْمِ حَتَّی یَطَأَ عَلَیْهَا رِضًا بِهِ.»

Hakika malaika hutandaza mbawa zao chini ya miguu ya mtafutaji wa elimu ili akanyage juu yake, kwa sababu wanaridhika naye. (2)

Ubora wa mwanachuoni juu ya mwenye kufanya ibada

Mtume Mtukufu (s.a.w.w) katika riwaya nyingine anasema:

«إِنَّ فَضْلَ اَلْعَالِمِ عَلَی اَلْعَابِدِ کَفَضْلِ اَلشَّمْسِ عَلَی اَلْکَوَاکِبِ.»

Hakika ubora wa mwanachuoni juu ya mwenye kufanya ibada ni kama ubora wa jua juu ya sayari nyingine. (3)

Kulinganisha saa moja katika utafiti wa kielimu na kumaliza Qur’ani mara elfu kumi na mbili

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) katika wasia wake kwa Abu Dhar walisema:

«یَا أَبَا ذَرٍّ اَلْجُلُوسُ سَاعَةً عِنْدَ مُذَاکَرَةِ اَلْعِلْمِ أَحَبُّ إِلَیَّ مِنْ قِرَاءَةِ اَلْقُرْآنِ کُلِّهِ اِثْنَیْ عَشَرَ أَلْفَ مَرَّةٍ.»

Ewe Abu Dhar! Kukaa saa moja mbee za majlisi ya elimu ni kwenye kupendeza zaidi kwangu kuliko kuisoma Qur’ani nzima mara elfu kumi na mbili. (4)

Kipaumbele mbele wino wa wanazuoni kuliko damu ya mashahidi

Aidha, Mtume Muhammad (s.a.w.w) amesema:

«إِذَا کَانَ یَوْمُ اَلْقِیَامَةِ وُزِنَ مِدَادُ اَلْعُلَمَاءِ بِدِمَاءِ اَلشُّهَدَاءِ، فَیُرَجَّحُ مِدَادُ اَلْعُلَمَاءِ عَلَی دِمَاءِ اَلشُّهَدَاءِ.»

Itakakapofika siku ya Kiyama, wino wa wanazuoni utapimwa pamoja na damu za mashahidi; ndipo wino wa wanazuoni utapewa uzito kuliko damu za mashahidi. (5)

Na kuna riwaya nyingi nyingine zinazodhihirisha ukubwa wa elimu na kujifunza.

Swali:
Inawezekanaje wino wa wanazuoni uwe bora kuliko damu ya mashahidi waliotoa kila walichokuwa nacho na kujitoa mhanga katika njia ya Mwenyezi Mungu?!

Jibu la swali hili liliulizwa kwa Imam Ma‘sumi, naye akasema:

“Yule anayeenda vitani kwa ajili ya jihadi hulinda mipaka ya nchi ya Kiislamu. Hilo huzuia maadui kuingia katika nchi ya Kiislamu na kuvamia mali, roho na heshima za Waislamu. Asipofanya hivyo, ardhi za Waislamu zitachukuliwa na makafiri, mali zao zitaporwa, na heshima zao zitahatarishwa. Jihadi haina matokeo yaliyo juu zaidi ya haya.
Lakini wale wanaokwenda kutafuta elimu — wao hulinda mipaka ya nyoyo za Waumini dhidi ya kuingia maadui na Shetani, ili wasiharibu imani yao na kuipora. Pale adui anapovamia na kuchukua mali ya mtu, hiyo ni hasara ya kidunia; Mwenyezi Mungu huilipa huko Akhera. Hata akiuliwa, amepoteza siku chache tu za maisha ya dunia, na Mwenyezi Mungu humpa maisha ya milele huko Akhera.
Lakini imani ya mtu ikiporwa — ni nini kitakachobakia? Adhabu ya milele!”

Ndiyo maana, kwa mujibu wa kauli tukufu ya Amirul-Mu’minin (a.s.):

“Elimu ni urithi wenye thamani kubwa.”

Rejea:
1. Nahjul-Balagha, Hikma ya 5.
2. Bihār al-Anwār, Juzuu ya 1, ukurasa 177.
3. Bihār al-Anwār, Juzuu ya 2, ukurasa 19.
4. Jāmi‘ al-Akhbār, Juzuu ya 1, ukurasa 37.
5. Amālī Sheikh Tūsī, Juzuu ya 1, ukurasa 521.
6. Ayatullah Misbah Yazdi, Hawza ya Delhi, Jumuiya ya Ahlul-Bayt (a.s.), Ijumaa, 4 Mehr 1382 Shamsia.

Imeandaliwa na Kitengo cha Elimu na Utamaduni cha Shirika la Habari la Hawza.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha